Thursday, September 28, 2006

Mtanzania Amkumbuka Nyerere Kwa Hisia Nzito

osted: Thu Sep 28, 2006 10:42 am Post subject: Barua kwa Mwalimu-By Nthelezi Nesaa

POSTED on KUMEKUCHA.COM forum

Mpendwa Mwalimu Nyerere,

Mbuya ori tata?
Katika kuadhimisha miaka saba tangu Marehemu Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere ututoke, nimeamua kufanya
hivyo kabla ya tarehe yenyewe kufika ili lau nikupe
nafasi ya kutafakari nitakayoyasema.

Kwanza Mwalimu watanzania wako bado wanakukukumbuka
sana hasa wanapopambana na matatizo ambayo wakati wa
uhai wako uliyatatua au kuyashiriki sawa na
wao.Wanaikumbuka falsafa yako ya usawa wa binadamu.
Kwa sasa kuna binadamu zaidi ya binadamu kutegemea una
nini na nafasi gani.

Tangu utuondoke Mwalimu watu wameanza kuona jinsi
ulivyokuwa na mapenzi ya dhati na ya aina yake kwa
nchi na watanzania. Kwani kama tulivyoambiwa kuwa
wakati ukikata roho ulikuwa unasema kuwa unawaacha
pabaya watanzania wako. Badala ya kumtaja mkeo mpendwa
Mama Maria na watoto wako, ulikuwa unawalilia
watanzania wako.

Hayo ni mapenzi yaliyotukuka kiasi cha kuwafanya
baadhi ya matapeli wa kidini kutaka sifa kwa kukutumia
eti wakutangaze mtakatifu. Wale uliowaacha laiti kama
wangefikia hatua ya kukata roho, wangesema "maskini
wawekezaji wetu tunawaacha pa baya"

Kitu kingine kinachofanya watanzania wakukumbuke ni
utabiri wako kutimia wakati ukikata roho kule Guy and
St. Thomas London tarehe ambayo haijulikani vizuri
mwezi wa kumi 1999.

Kama wahenga walivyowahi kusema kuwa si ajabu panya
wakala viatu hata ngao ya shujaa maarufu kwa uuaji wa
simba. Kwani tangu uondoke, wale ulioamini kuwa
uliwafundisha wakakuelewa kumbe siyo, waliigeuza nchi
chaka la wezi.

Nguchiro, vinyamkera, vicheche na vinyama vyote vya
usiku vilivamia nchi iliyokuwa ya watu na kuigeuza
nchi ya wanyama. Yale maonyo yako kuwa Ikulu ni sehemu
takatifu yalionekana upuuzi kwao.

Kwanza tangu uondoke shilingi Bilioni tatu
zilishatumika kuitia mkorogo Ikulu ukiachia mbali
ulaji na matumizi mengine mabaya juu ya ununuzi eti wa
mashine za kuditekti moto!

Mwalimu sijui katika kuzinunua walitumia kiasi gani
lakini najua kuwa Mungu aliwaumbua baada ya kutenda
dhambi ile. Maana chumba cha Rais kiliungua wakati
yeye na mkewe wakiwa nje wakitanua. Hatujui kama hata
kwenye hekelu lao la kule Lushoto nako wameweka
manjonjo haya.

Pia tangu uondoke matumizi mabaya yamekuwa ndiyo
mtindo wa maisha. Kwani kuna mdege mkubwa ya kisasa
amenunuliwa Rais baada ya wananchi kupinga kuwa ni
aghali sana. Unaitwa Gulf stream na hauwezi kutua
kwenye viwanja visivyo vya kisasa kama wenyewe. Ili
ujue hali ilikuwaje, Mwalimu bado nadhani unakumbuka
kuwa kipindi fulani washamba wetu walikuwa
wanashindana kununua mipete ya dhahabu na mikufu
utadhani ni akina Defao. Kwa ushamba wao hawakujua
kuwa mikufu ya Tanzanite na almas wanavyochezewa
ndivyo mali kama wakiamua kuwa malimbukeni.

Mwalimu wahenga waliwahi kusema kuwa simba aweza kuzaa
mbwa. Haya ni kweli tangu uondoke. Kwani wale
tuliowaamini kutokana na wewe kutuambia kuwa ni
wasafi, walikuangusha vibaya wakageuka vibaka na
manyang'au walioshirikiana na watu wanaoitwa
wagenishaji na wawekezaji kuiibia nchi yetu. Wakati
wakiingia tuliwajua kama mabwana na mabibi wasafi
lakini wakati wa kutoka wameondoka wakiwa mabingwa wa
uchafu tena waliondoka kimya kimya hata bila kuaga!
Wangemuaga nani iwapo hata inzi walikuwa wakiwazomea?

Kwa mfano, wao na mashemeji wao waliiweka rehani
TANESCO. Ilipoingia serikali mpya ambayo samahani kuwa
nilikuwa sijakuelezea kuwa kuna Rais wa nne, nayo
serikali mpya inataka kuleta Makampuni wake wa Kigeni.
Hii haikuingia na uwazi na ukweli bali kasi mpya nguvu
mpya na ari mpya lakini kwa bahati mbaya wasaidizi wa
jenerali wa batiani hii ni re-cycled sometimes or
completely re-cycled.

Hao waliokuwa wamekopa TANESCO kujua hivyo waliamua
kufungulia maji yote kwenye mabwawa kiasi cha
kusababisha ukame wakati wa masika.

Hivyo Mwalimu kama ulivyotabiri, watanzania wanaishi
kama nungunungu au popo kwenye kiza takriban kwa mwaka
huu wote. Majenereta yanafuka moshi na kupiga mikelele
utadhani Baghdad.

Wahenga mwalimu walisema kuwa kutu hutafuna chuma.
Najua kuwa uliacha marehemu NBC, DAHACO hata baadhi ya
migodi vikiwa vimeishapigwa mnada. Nakumbuka
ulivyokinusuru kiwanda cha nguo cha URAFIKI
kisinyakuliwe na manyang'au na wakora.

Sasa Mwalimu huwezi kuamini kinachoendelea kwani hata
pale Musoma watu wameishapigwa risasi na kufa! Ya
Bulyankhulu uliayaacha. Kisa eti wanakatiza au
kujitafutia riziki kwenye sehemu zinazomilikiwa na
wawekezaji.

Mwalimu, huwezi kuamini kuwa hata wale uliowabwatukia
kuwa wamejilimbikizia mali za wizi ambazo hawawezi
kuzitolea maelezo sasa ndiyo viranja na manabii wa
kuwahubiria watanzania wako injii ya watawavusha na
kuwafikisha Kanani! Wenye akili wameishaanza kuonya
kuwa huu ni mvinyo ule ule bwate lile lile au kanzu
mpya lakini shehe yule yule.

Kwa sasa viranja ambao wengi wao uliwasomesha kwa pesa
ya mlipa kodi kutokana na wazazi wao kuwa makapuku, ni
mabilionea wenye harufu ya utajiri na ukwasi utokanao
na ujambazi na umalaya wa kiuchumi.

Kitu kingine Mwalimu ni kwamba zile nyumba
ulizowanyang' anya majambazi wa kiuchumi pale mwaka
1967 zimeishatokomea. Kwani wale manyang'au si
walizigawana na kuanzisha upuuzi mwingine eti kujenga
nyumba za watumishi wa serikali.

Mwalimu namshukuru Mungu kwani alikupenda mno na
kukulindia heshima kwa kukuchukua mapema ili
usishuhudie makufuru yaliyofanywa na wale uliodhani
kuwa ni watu kumbe ni aina ya wanyama waitwao
masupials. Wao na wake zao ni watu wa kutanua kwani ni
matajiri kwa kutupwa. Watoto wao wanatanua ughaibuni,
wakiugua mafua wao hata hawara zao hupelekwa majuu
kupima hata mafua na uchovu wa kawaida.

Kama kuna sehemu Mwalimu walikudhalilisha si kwingine
bali kwenye msiba wako. Maana walitumia jina lako na
kulinajisi. Eti walitwambia kuwa walitumia shilingi
Bilioni moja na ushee kwa ajili ya mazishi yako
utadhani ulikuwa Bilionea au mfalme.

Walikutumia kutuibia pesa maana tunakujua ulivyochukia
makuu ungekuwa hai usingekubali isirafu hii hata huu
utakatifu wa kuchongwa unaotaka kupewa.

Kabla sijasahau Mwalimu, kumbe ni kweli kuwa paka
akiondoka mipanya hujitawala. Kwani baada ya kuondoka,
ule mpapure uliotuachia uliota mabawa baada ya kunywa
kwenye kombe la madaraka. Najua Mwalimu ulipenda
kuchanganya na umombo kwenye hotuba zako. "Do you know
what? The dugong-like thing played God and holier than
thou to commit all buffoonery" The guy brought his
gang of goons and kit of caboodle of devils in the
sacred place. The holy of the holy was defamed God
knows Mwalimu.

Wapo vijana waliojaribu kuhoji hii Infallibility and
corruption, unajua waliambiwaje? "Nyinyi ni wavivu wa
kufikiri. Kwanza mna wivu wa kike. Basi kama
hamnisifii wafadhili watanisifia" Huwezi kuamini
Mwalimu kuwa utumbo huu ulisemwa na mtu aliyewahi
kuingia kwenye darasa lako! Lakini ilitokea huu ndiyo
ukweli. Kuwa kumbe ulikuwa unaishi na kulea michui
iliyokuwa imevaa ngozi ya fisi.

Enhee! Mwalimu ule Muungano uliouasisi mwaka 1964 kwa
sasa umebaki kama kichekesho. Kwani serikali ya
mapinduzi ya jimbo la Zanzibar hivi karibuni ilitoa
amri ya kuwataka wabara kuwa na vibali kuingia huko.
Huwezi kuamini kuwa hata kwenye uchaguzi wa 2005,
wakati mtoto wa Rafiki yako aking'ang'ania kuendelea
kukalia ulaji, wanajeshi na polisi waliwapiga
watanzania wako kile kipigo cha mbwa mwizi.

Najua wewe hukupenda cheo ambacho ni dhamana kurithiwa
na mtu ndiyo maana hakuna mwanao uliyemuandaa kuwa
mwanasiasa.

Usishangae siku moja nikakuletea salamu toka nchi ya
Tanganyika, Pemba na Zanzibar. Wala Mwalimu usishangae
ukisikia msamiati wa Wazanzipemba, Wazanziafrika na
wazanziarabu.

Pia Mwalimu katika uchaguzi huo chama chako cha
Mapinduzi kulipewa sifa na majina lukuki. Kwani
kiliitwa chama cha Matajiri, Majambazi hata
magabacholi maana pesa zilimwagwa kama njugu. Kumbe
ule utabiri wako kuwa kuna kipindi Rais wa nchi
ataamuliwa na mfuko wake. Hatusemi kuwa ilikuwa hivyo
japo ndo hiyvo hivyo, ni kwamba uchanguzi huu ulikuwa
ni matanuzi si kawaida.

Hatujui hadi leo nani alimnunua nani kati ya watawala
wetu na washitiri wao na wapiga kura wetu! Mwalimu si
uliacha migodi ishapigwa mnada tena kwa bei ya "Tajiri
leo kapata kichaa anagawa bure".Kwa taarifa zilizopo
ni kwamba hata mbuga za wanyama na misitu na mapori
hata vichochoro vya Msasai kama wawekezaji watavitaka
vitauzwa kama utawala uliopo nao utaendekeza ulevi wa
madaraka.

Sisi tunasema watauza hadi kaburi lako Mwalimu kama
hawatajitofautisha na wale waliofanya makufuru yote
tuliyokusimulia.
Enhee Mwalimu, pia tukukumbushe kitu kingine muhimu.
Wewe ulishutumiwa kuwa ulibana uhuru wa vyombo vya
habari. Afadhali yako maana kwa sasa huwezi ukajua
vyombo vya habari viko wapi. Waandishi siku hizi
wanaukwaa ukuu wa mkoa hata wilaya. Hii ni baada ya
kutembeza kampeni hadi mtu wao kupita. Maadili ya
vyombo vya habari hakuna.

Kwani kama waandishi wapewavyo mishiko midogo ya elfu
tano, waandamizi wanapewa maulaji ya vyeo. Hayo
tuyaache. Ili tusikuchoshe sana, ndiyo maana
tumekukumbuka mwezi mmoja kabla ya siku yenyewe ili
uwe unajisomea taratibu.
Pia nisisahau miaka kama miwili iliyopita, ilifikia
mahali hotuba zako marehemu zikawa na mantiki na akili
kuliko viumbe waliokuwa hai wakitangaza injili ya
ubinafsishaji, ujambasishaji, ugenishaji,
ushemesishaji.

Kwanza walijifanya mabingwa wakawa wanaandika mihotuba
mirefu, kavu na yenye ukali utadhani walikuwa
wakihutubia wafungwa.

Mwisho, ukimwi bado unaua. Ila ajabu Mwalimu si unajua
wale TACAIDS. Basi Mwalimu wao wanachofanya ni kununua
mishangingi ya bei mbaya, kuandaa masemina kwenye
mahoteli ya kifahari na kupiga picha za Makete na
kusambaza na kupata mshiko huku watu wanateketea.

Mwalimu ile ajali ya kisiasa uliyokuwa ukitufundisha
pale Pugu kumbe ilikuja kutokea ambapo wananchi
walijuta na kusaga meno. Maana ilitokea hata watu
wakaanza kuamini kuwa kumbe mtaua aweza kuzaa jambazi
na bikira kuzaa kahaba!

Kwa vile ulikuwa mtu wa kimataifa, hatuwezi kumaliza
barua yetu bila kukupa lau salamu kidogo. Mzee Mandela
na Rafiki yako Kenneth ni wazima. Yule rafiki yako wa
zamani Obote na hasimu wako Amin waliishakufa.

Pia kule Malawi yule Rais mfanyabiashara Bakili
aling'olewa kwa aibu kama Chiluba walipong'ang' ania
kunya sorry kuchafua katiba. Charles Taylor, yule
jambazi wa kimarekani si unamkumbuka? Yuko ananonihino
kwenye debe. Walimwengu wanawangojea majambazi wengine
kama Meles Zenawi, Yoel Museveni, Paulo Kagame,
Theodore Obiang Ngwema, Dennis Sassou Ngweso, Omar
Bashir na Yahaya Jammeh.

Kule Rwanda yule Rais Kibaraka aitwaye Pasteur
Bizimungu aliishapinduliwa na mfalme Paul Kagame wa
ukoo wa kifalme wa MUSEVENI ndiye anatawala akitumia
vitisho na kutunza mafuvu ili dunia imuonee huruma na
kumchukulia kama mtu aliyeituliza ile nchi ilhali
ndiye alifanya mauaji ya marais watatu.

Pia Marekani ilizivamia Afghanistan na Irak
ikazipindua na inaendelea kuzikalia. Ila nayo sasa
inajuta maana inapokea kipigo cha mbwa sawa na
watanzania wako kule Zanzibar.

Mama Maria ni mzima hata vijana wako nao pia.
Watanzania hao maskini hawana uzima wowote zaidi ya
kuishi kwa matumaini tu. Mzee Mwinyi naye ni mzima ila
mvi zinamsumbua sana. Rashid hajambo jambo japo haishi
kulazwa. Kingunge bado anaendelea kuwa kijana maana ni
waziri! Hata John yupo na siku hizi amepoa si haba ila
Ben amejificha sana maana alichowafanyia watu wako
sijui!

Mwlimu naona kwa taadhima na unyenyekevu nikuage
nikikutakia mapumziko mema.
Wasalimie Kwame Nkruma, Patrick Lumumba,Modibo Keita,
Obafemi Owolowo, Nnandi Azikiwe,Ken Saro Wiwa, Gamal
Nasser, Oliver Thambo, Walter Sisulu, Govan Mbeki,
Steve Biko, Seletse Khama,Augustino Netto, John Garang
de Mabior na mashujaa wengine uwajuao.

Hizo ndizo habari za huku Mwalimu.
Ni Binti yako akupendaye daima na watanzania wako
Nthelezi Nesaa

No comments: