Saturday, 29 November 2008
KIKWETE AFANYA MABADILIKO (MAKATIBU WAKUU)
Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa makatibu wakuu wapya, kuhamisha wengine na kuteua manaibu katibu wakuu wapya. Kwa sasa, Mgonja ambaye yuko katika likizo ya kustaafu, amestaafu sambamba na makatibu wakuu wengine watatu na Naibu Katibu Mkuu mmoja kati ya Agosti na Novemba mwaka huu. Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo katika taarifa yake Dar es Salaam jana, aliwataja wastaafu wengine ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Vincent Mrisho, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Abel Mwaisumo, Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bakari Mahiza na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Charles Sanga. Luhanjo alisema kutokana na kustaafu kwa makatibu wakuu na Naibu Katibu Mkuu huyo, Rais Kikwete amefanya uteuzi na uhamisho wa makatibu wakuu na baadhi ya manaibu makatibu wakuu. Aliwataja makatibu wakuu wapya ambao wote walikuwa ni manaibu katibu mkuu ni Ramadhani Khijjah anayemrithi Mgonja, awali akiwa Naibu Katibu Mkuu Hazina. Wengine ni Dk. Florens Turuka anayekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, akitokea Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko; Joyce Mapunjo anayekwenda Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, akitokea Maendeleo ya Miundombinu na Andrew Nyumayo kusimamia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, akitokea Ofisi ya Waziri Mkuu. Aliwataja Manaibu Katibu Wakuu wapya kuwa ni Dk. Phillip Mpango (Wizara ya Fedha na Uchumi) ambaye awali alikuwa Msaidizi wa Rais (Uchumi)-Ikulu, Selestine Gesimba (Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi), akitokea Mkurugenzi wa Sera na Mipango ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Mwingine ni Seti Kamuhanda anayekwenda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Awali alikuwa Msaidizi wa Rais (Hotuba) Ikulu; na kabla ya hapo, alikuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), inayochapisha Daily News, Sunday News, HabariLeo na HabariLeo Jumapili. Katika uhamisho huo, Luhanjo aliwataja waliohamishwa na sehemu wanazotoka na wizara walizopangiwa katika mabano kuwa Peniel Lyimo (Ofisi ya Waziri Mkuu kutoka Kilimo, Chakula na Ushirika); Dk. Ladislaus Komba (Maliasili na Utalii kutoka Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana) na Kijazi Mtengwa (Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kutoka Habari, Utamaduni na Michezo. Wengine ni Mohammed Muya (Kilimo, Chakula na Ushirika kutoka Mambo ya Ndani; Patrick Rutabanzibwa (Mambo ya Ndani kutoka Maji na Umwagiliaji); Dk. Stergomena Tax (Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Viwanda, Biashara na Masoko); Wilson Mukama (Maji na Umwagiliaji kutoka Afya na Ustawi wa Jamii); na Blandina Nyoni (Afya na Ustawi wa Jamii kutoka Maliasili na Utalii). Aidha, Luhanjo alisema rais amemhamisha Naibu Katibu Mkuu Fanuel Mbonde kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu. Katibu Mkuu Kiongozi alisema uteuzi wa makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu hao unaanza mara moja.(Source - Colleague's blog)